Katika kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kutoa huduma kwa kadri ya matarajio ya wengi tarehe 15/02/2016 Mhe. Selemani Jaffo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alifanya ziara katika Soko la Samaki Feri.

Katika Ziara yake Mhe. Jaffo alitoa maelekezo kwa Uongozi wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha kuwa kero zilizopo katika soko hilo zinatatuliwa ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja kwani aliahidi kurudi sokoni hapo tarehe 15/03/2016 kufuatilia utekelezaji huo.

Miongoni mwa kero ya muda mrefu iliyokuwepo ni kukosekana kwa Bodi ya Soko suala ambalo alihakikishiwa na Uongozi wa Manispaa kutatuliwa ndani ya muda huo kufuatia kuidhinishwa kwa matumizi ya Sheria ndogo za Soko  za Uendeshaji wa Soko la Samaki Feri.

Kwa upande wa mapato Mhe. Naibu Waziri aliagiza kuwa kila eneo la ukusanyaji sokoni hapo litumie mashine za kielektroniki na kueleza kwamba Soko la Samaki Feri ni mojawapo ya chanzo cha mapato kinachotegemewa.

Aidha alipongeza jitihada zinazochukuliwa za kuliweka soko katika Hali ya Usafi. Maagizo mengine aliyoyatoa ni pamoja na kurekebishwa kwa Chemba ya maji taka na kuanza kufanya kazi kwa majiko yatakayotumia mfumo wa gesi.